Na,Jumbe Ismailly -Mkalama May,18,2015 Kuchafuana
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Mkalama kimekemea tabia ya baadhi ya wanachama wake wenye nia ya kutaka kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao wa Rais,wabunge na madiwani baadaye mwaka huu kuacha mara moja kuanza kuwachafua viongozi waliopo madarakani.
Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Mkalama,Elipendo Machafuko alipokuwa kifungua kikao cha baraza la jumuiya hiyo wilayani Mkalama,mara tu baada ya kumpokea Mbunge wa viti maalumu (CCM) Mkoa wa Singda,Mather Mlata aliyekuwa na ziara ya siku moja wilayani hapa.
Kwa mujibu wa Machafuko wakati wakielekea kwenye uchaguzi mkuu mwezi oktoba,mwaka huu kumeanza kujitokeza wingu la watu wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kuanza kuwachafua viongozi waliopo madarakani,jambo ambalo linaweza kuleta mfarakano ndani ya chama.
“Tunaenda kwenye mchakato wa uchaguzi,liko wingu la kuchafuana sanaa..kama unamchafua Mather Mlata bado yupo madarakani,hivi wewe ukichafuliwa utafurahi,utatabasamu,ukimchafua mwenyekiti wa Halmashauri wakati bado anatawala kule Halmashauri atafurahi,iko hii tabia,ipoo?alihoji mwenyekiti huyo wa UWT Mkalama.
Akizungumza na wajumbe wa baraza la UWT wilaya ya Mkalama,Mbunge wa viti maalumu (CCM) Mkoa wa Singida,Marther Moses Mlata alisema demokrasi ndani ya Chama Cha Mapinduzi ni ya kujivunia sana kwani inampa nafasi kila mwanachama kugombea,kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi yeyote ya uongozi.
“Jamani ndani ya chama cha mapinduzi kuna demokrasia,simmeona watu wengine demokrasia hamna sasa hivi tu mnyukano,sisi kuna demokrasia inapofika wakati watu wanajitokeza ili watu wawapime,watu wachaguliwe”alisisitiza Mlata
Hata hivyo Mlata ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la UWT Taifa aliwaweka wazi wanachama wa jumuiya hiyo kuwa yeyote yule mwenye nia na uwezo wa kuwatumikia wananchi wa Mkoa huo wakati ukifika wajitokeze kuchukua fomu na kujaza ili waombe nafasi zitakazotangazwa na chama.
Naye katibu wa UWT Mkoa wa Singida,Angela Robert Milembe alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha watendaji wa jumuiya hiyo kwamba msaada wa vitendeakazi vilivyotolewa na Mbunge Mlata visije vikawa chanzo cha kuwafarakanisha na badala yake viwazidishie umoja na mshikamano zaidi.
Awali katibu wa CCM wilaya ya Mkalama,Amosi Shimba akimkaribisha Mjumbe huyo wa Baraza la UWT Taifa aliwahakikishia wajumbe na wanachama wa chama hicho kwamba misaada hiyo iliyotolewa na mbunge huyo siyo rushwa bali anatekeleza ilani ya chama tawala.
“Kwa sababu mbunge aliyepo madarakani anayoyafanya siyo rushwa,niombe kutoa wito kwa viongozi wengine mliopo madarakani,msipate kigugumizi,msisite,kukisaidia chama kijipange kujiandaa kwenda kwenye mchakato,mama Mlata kila la kheri”alisisitiza huku akishangiliwa na wajumbe waliohudhuriaa kikao hicho.