" Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa
Bunge Maalum la Katiba; Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi; Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania; Mheshimiwa Maalim Seif Sharif
Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar; Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi,
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa
Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa
Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania; Mheshimiwa Othman Makungu,
Jaji Mkuu wa Zanzibar; Viongozi Wakuu
Wastaafu; Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba; Waheshimiwa Wajumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba; Wageni
waalikwa; Mabibi na Mabwana; Pongezi
Nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti
kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge letu
Maalum la Katiba katika siku hii muhimu na
ya kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja
kuwatakia heri na naungana na Watanzania
wenzetu wote kuwaombea baraka za
Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi
yenu kwa utulivu, hekima, umakini mkubwa
na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio
yanayoyatarajiwa na Watanzania. Natoa
pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako
kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge hili
maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa
mliopata ni kielelezo tosha cha imani kubwa
na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu
kwenu. Matumaini yao ndiyo matumaini ya
Watanzania wote, kwamba mtaliongoza vizuri
Bunge hili, ili liweze kutimiza kwa ufanisi
mkubwa jukumu lake muhimu sana katika
historia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Mheshimiwa Mwenyekiti; Niruhusu
pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa
Bunge Maalum la Katiba kwa bahati ya aina
yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Fursa
hii hutokea mara chache sana katika historia
ya nchi yo yote na watu wake. Mkifanikiwa
kuipatia nchi yetu Katiba nzuri majina yenu
yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika
kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Ni matarajio ya
Watanzania kuwa mtatunga Katiba
itakayokubalika na wengi. Katiba
inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha
Muungano wetu kwa kuondoa changamoto
zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu
mfumo bora wa kuongoza na kuendesha
mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja,
upendo, ushirikiano na mshikamano
miongoni mwa wananchi wa Tanzania, licha
ya tofauti zao za asili za upande wa
Muungano na maeneo watokako, au tofauti
za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa
vyama vya siasa. Katiba itakayodumisha
amani, usalama na utulivu nchini. Katiba
itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za
binadamu, utawala wa sheria, utawala bora
na kudhibiti maovu. Na, mwisho ingawaje
siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba
itakayoweka mazingira mazuri kwa uchumi
wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika
sawia na maendeleo yatayopatikana. Historia
ya Katiba Nchini Mheshimiwa Mwenyekiti na
Waheshimiwa Wajumbe; Hii itakuwa mara ya
tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964, kwa
nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga
Katiba mpya. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka
1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara
ya pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya
Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti na mara
mbili zilizopita, safari hii mchakato
unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi
wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao
kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na ndio
watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu
Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi
pia walipata nafasi ya kuchagua Wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili
Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata
nafasi ya kutoa maoni yao kupitia Mabaraza
ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo
wananchi 201 kutoka makundi mbalimbali.
Katika mchakato wa kutunga Katiba za
mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za
Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum la Katiba
kama ilivyo katika mchakato huu. Hata hivyo,
kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano pekee ndio waliounda
Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum
linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi na wananchi 201 wanaotoka
kwenye jamii, wakiwakilisha asasi na
makundi mbalimbali ya Watanzania kutoka
Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa
sasa utaishia kwenye kura ya maoni
itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania
wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato
iliyopita iliishia Bunge Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili,
1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa
mabadiliko takriban mara 14. Mabadiliko
hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa
mabadiliko muhimu ya kiuchumi, kisiasa na
kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini
na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje baadhi ya
mabadiliko yaliyofanywa:-
1. Mabadiliko ya 1979 yaliunda Mahakama
ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa
Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki
baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki mwaka 1977. 2. Mabadiliko ya
mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa
kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo kulazimu
Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya
Jamhuri ya Muungano. 3. Mabadiliko ya
mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo
wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo kabla
ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za
Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa kwa
mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile,
Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mambo
mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya
Mambo ya Muungano. 4. Mwaka 1992,
yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo
wa Vyama Vingi vya Siasa badala ya ule wa
Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia
utaratibu wa uchaguzi wa Rais na Wabunge
ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa
vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa
kuwa na viti maalum vya wanawake katika
Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa
asilimia 15 ya Wabunge wote. Aidha, kwa
mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu
Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha
Rais na Waziri Mkuu kupitia kura ya
kutokuwa na imani. 5. Mabadiliko ya mwaka
1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata
Makamu wa Rais kupitia Mgombea Mwenza.
6. Mwaka 2000 na 2005, pamoja na mambo
mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua
wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza
uwakilishi wa wanawake. Umuhimu wa
Mabadiliko ya Katiba Mheshimiwa
Mwenyekiti; Kufanyika kwa mabadiliko hayo
kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya
mabadiliko kila ilipoonekana inafaa kufanya
hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo na
Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo
na madai yaliyokuwa yanajirudia ya kutaka
Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako
watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo
yenye viraka vingi mno kiasi kwamba ingefaa
kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai ya kutaka Katiba mpya yalipazwa
sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama
vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai
Katiba mpya kwa imani, eti kwamba,
itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo
tu, hata katika mchakato wa Serikali zetu
mbili kushughulikia kero za Muungano,
imedhihirika kuwa baadhi ya changamoto
zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya Katiba ili
kuzipatia ufumbuzi wa uhakika na wa
kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa kutambua
ukweli huo na baada ya kushauriana na
kukubaliana na viongozi wenzangu wakuu wa
Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati
ule, ndipo tarehe 31 Desemba, 2010,
nikatangaza dhamira ya kuanzisha mchakato
wa kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile
kuwa katika mchakato huo tutakuwa na
ushirikishwaji mpana wa wananchi wa
Tanzania kwa makundi yao ya jinsia, dini,
siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki
na kwa maeneo wanayotoka katika pande
zetu mbili za Muungano. Mchakato wa
Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti; Tarehe 16 Machi,
2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa
kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya
kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria hiyo,
mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa
unaanza kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la
kusikiliza maoni ya wananchi mmoja mmoja
na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao
na kupitia Mabaraza ya Katiba. Mwishowe
Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya
Katiba mpya itakayofikishwa kwenye Bunge
Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya
kutungwa. Mchakato wa Katiba
utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya
maoni ya kuamua kama wanaikubali au
kuikataa Katiba mpya. Tarehe 6 Aprili, 2012
nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kuwaapisha tarehe
13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2
Mei, 2012 na kuikamilisha kwa mafanikio,
hatua zote zilizoihusu na kukabidhi kwangu
na kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na
Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013.
Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume,
Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha
Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu
tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi
kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi
inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili, kuamua
na kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo
Katiba mpya itafikishwa kwa wananchi kwa
uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura
ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Rasimu ya Katiba
ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na
magazeti mengine yanayosomwa na
wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu
cha 20(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na
Rasimu ya Katiba viliwekwa wazi kwenye
tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma.
Inafurahisha kuona kuwa watu wengi
wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu ya
Katiba na kumekuwa na mjadala mpana
kuhusu nyaraka zote hizo muhimu. Watu
wengi wametoa maoni yao na wanaendelea
kufanya hivyo. Kwa maoni yangu hili ni
jambo jema sana na ni kielelezo thabiti kuwa
demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi
Tanzania. Pia, kwamba, Watanzania wako
huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa
mambo yanayowahusu. Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa mara nyingine
tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph
Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji
Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa na
nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi
hasa ukizingatia ukubwa wa nchi yetu, wingi
wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la
kumpoteza Mjumbe mwenzao muhimu Dkt.
Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya haki
katikati ya mchakato. Pamoja na hayo, kwa
bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza
kutembelea mikoa yote nchini na kuwafikia
watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa
mdomo na kwa maandishi. Halikadhalika,
walipokea na kuchambua maoni 772,211
kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali.
Baada ya kupokea maoni ya wananchi,
kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na
uzoefu wao, Wajumbe wakafanya kazi ngumu,
kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba
iliyoko mbele ya Bunge hili. Ni kweli kwamba
Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi
wote wa Tanzania, lakini wameweza
kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa kiasi
kikubwa wanawakilisha taswira na mitazamo
mipana ya jamii yetu. Baadhi ya Masuala
Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa
Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti; Tume imefanya kazi
nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa
kwa taifa la Tanzania. Rasimu imeandikwa
vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume
imetoa mapendekezo ambayo kwa kiasi
kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba ya
nchi yetu, kwa namna ya pekee. Katiba
inayopendekezwa, imejumuisha dhana na
mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema
na wakati tulionao na kuweka msingi mzuri
kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu za
kawaida za marekebisho ya Katiba
tuliyonayo, isingekuwa rahisi kuingiza
mambo mengi mapya kiasi hiki. Wajumbe
Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti; Waheshimiwa
Wajumbe; Rasimu ya Katiba ni kitabu
kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina
kurasa 106, sura 17 na ibara 271. Wajumbe
wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa
vizuri kila kilichoandikwa ili muweze kufanya
uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika kuchambua
kwa kina na umakini mkubwa kila kilichomo,
sura kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa
sentensi na hata neno kwa neno. Hamna
budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu
vya Rasimu ya Katiba na kufaa kwa dhana
mbalimbali zilizoingizwa na kujengeka katika
Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kile ambacho
Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au
kurekebishwa au kufutwa msisite kufanya
hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo
bora. Msipofanya hivyo kuna hatari ya
kupata Katiba ambayo ni ngumu kuitekeleza.
Aidha, tunaweza kuwa na Katiba ambayo
itanung’unikiwa na watu wengi na
kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe
marekebisho muda mfupi baada ya
kupitishwa. Bunge hili linao wajibu maalum
wa kuzuia balaa hilo lisitokee katika nchi
yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa katika
mchakato huu ni kama chujio la kuepusha
hali hiyo isitokee. Kile ambacho
hakikuonekana katika hatua moja
kitaonekana katika hatua inayofuata na
kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo
muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Nimekwishaeleza
kuwa moja ya jambo mnalotegemewa
kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya
kutunga Katiba ya nchi yetu ni kujiridhisha
na uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa
kuhusu uandishi ambayo naomba
myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa
mfano, kuna baadhi ya vifungu vya Katiba
vinayopendekezwa vimekuwa na mambo
mengi mno kuliko inavyostahili Katiba kuwa
(too prescriptive). Pia kuna mawazo kwamba
baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa
katika Katiba bali yawe kwenye Sheria
zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako mambo yaliyotajwa kwenye Katiba
ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu
hatakwenda mahakamani kuidai Serikali
impatie (non justiciable). Mambo yaliyotajwa
kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini
lazima yaendane na uwezo wa nchi na
uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba
tuyatoe kwenye Katiba, bali yabakie kama
dhamira pale uwezo wa nchi utakaporuhusu
yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari
ya Serikali kujikuta inalaumiwa au hata
kufikishwa mahakamani kila wakati kwa
madai ya jambo moja au jingine ambayo
haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo
kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na
Katiba ambayo ni ngumu kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Yapo pia maoni
kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu katika
uandishi wake, hivyo kuhitaji kufanyiwa
marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza
kuwepo athari na nyingine zinaweza kuwa
mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu
inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi
yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa “Eneo la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo
lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake
ya bahari na eneo lote la Zanzibar
likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo hayo yameacha kutambua, kwa
upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya
maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa
nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi kwa
nchi tunazopakana nazo siku moja wakaja
kupora sehemu zetu hizo na sisi kukosa
utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu
haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu?
Hili ni jambo kubwa ambalo Bunge hili
lazima mlirekebishe. Wakati ndiyo huu
hakuna mwingine. Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo jingine kuhusu uandishi ni mgongano
kati ya pendekezo la msingi la Tume la kuwa
na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya
Serikali ya Muungano ambayo kimsingi ni
majukumu ya Serikali za nchi washirika.
Katika Rasimu hii malengo ya taifa
yameainishwa na Serikali ya Muungano
inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo
yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni. Katika
mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na
Tume masuala yahusuyo uchumi na
maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo,
ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo,
elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika yako
chini ya mamlaka ya Serikali za nchi
washirika. Mamlaka ya Serikali ya Muungano
ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na
Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na
Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na
Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya
Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa
Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo
na Mambo ya Muungano. Kwa Rasimu
kupendekeza muundo wa Serikali tatu na
kuipa Serikali ya Muungano majukumu
ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha
utata na migongano kati ya Serikali ya
Muungano na nchi washirika. Mkichagua
mfumo wa Serikali tatu, inawalazimu
muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya
Muungano haistahili kuyatekeleza na wala
haina uwezo wa kuweka masharti kwa
Serikali za nchi washirika kwa mambo yaliyo
kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini kama
mtaamua tuendelee na muundo wa Serikali
mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na
Serikali ya Muungano bila ya matatizo.
Katika uandishi wa Rasimu Utumishi katika
Serikali ya Muungano haumo katika Orodha
ya Mambo ya Muungano. Ni lazima liwemo.
Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo
uandishi katika Rasimu. Naamini mkiisoma
Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua
mengineyo. Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti; Katika Rasimu kuna
dhana mpya na mambo mapya kadhaa
yaliyoingizwa ambayo yanabadili utaratibu
wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo
mbalimbali. Nawaomba mfanye uchambuzi
wa kina kwa kila kinachopendekezwa na
kujiridhisha kuhusu kufaa kwake na manufaa
yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo
kwa mambo mazuri na uendeshaji mzuri wa
shughuli katika taifa letu changa. Mambo ni
mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza
kuyazungumzia yote. Niruhusuni nizungumzie
baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo
katika Rasimu. Jambo la kwanza, kwa mfano,
linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana
ya “Mbunge kupoteza Ubunge iwapo
atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa
miezi sita mfululizo kutokana na maradhi au
kizuizi ndani ya gereza”. Watu hawana tatizo
na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza
kama amepatikana na hatia Mahakamani na
kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko
rumande kwa tuhuma akisubiri kesi
kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia
na kuachiliwa? Naungana na wale
wanaoshauri kuwa jambo hili lifafanuliwe
vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani
na kupata adhabu ya kifungo cha kipindi
hicho. Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa
mikanganyiko. Hakuna haja ya kusubiri
mpaka jambo hili lije kufafanuliwa baadaye
kwa Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa upande wa mtu
kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua
kwa miezi sita mfululizo” ni maoni ya watu
wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili
kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo
ubinadamu na wakati mwingine Mbunge
anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi
wa Jimbo lake. Anaweza kuugua kwa miezi
sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi
chake cha Ubunge kufika mwisho. Kwa nini
awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya
mwaka 1977 tunayotumia sasa haina sharti
hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya kuwa
na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi?
Wanasema kwa kweli anachostahili Mbunge
huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake
iimarike ili aendelee kutumikia watu wake, na
siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie watu
kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa
sharti hilo. Ni vyema jambo hili mkalitazama
kwa makini, na muone kama linastahili
kuwepo au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Katika Rasimu hii
imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo
wa vipindi vitatu kwa Wabunge. Tena
mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu
mfululizo au la!. Jambo hilo limezua mjadala
motomoto katika jamii. Ni vizuri
mkajiridhisha juu ya sababu za msingi na
manufaa ya kufanya hivyo hapa Tanzania.
Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni
kuweka ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa
sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini,
kuwawekea ukomo Wabunge ni jambo jipya
na huenda Tanzania tukawa wa kwanza.
Nashawishika kuungana na wale
wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema
mno kuanzisha utaratibu huo hapa kwetu.
Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya
kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri
wa uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa
nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu za
msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Jambo lingine jipya
linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa
kumuondoa Mbunge katikati ya kipindi chake
cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa
jambo jema lakini naomba athari zake
mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha
misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha
Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu bali
wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao
kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu
unaopendekezwa wa Chama chake kujaza
nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika
mazingira hayo nao unaweza kuwa ndicho
kichocheo kikubwa cha vuguvugu la
kumuondoa Mbunge. Walioshindwa kwenye
kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya
kuwachimba wenzao mpaka waondoke.
Jipeni muda wa kupima faida na hasa
thamani inayoongezwa na kuanzisha
utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama
jambo hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi
kila miaka mitano kurudi kwa wananchi
hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu
wamemchoka? Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti; Jambo lingine
kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo
limevuta hisia za karibu watu wote nchini
linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa
wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Pendekezo hili limezua mjadala mkubwa
tangu lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza
na kurudiwa katika Rasimu ya pili. Wakati
mwingine mjadala umekuwa mkali na wa
hisia kali kwa kila upande. Kwa kweli hili
ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu
kwa sababu linapendekeza kuanzishwa kwa
muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi
yetu. Hii ndiyo agenda mama ya Bunge hili
ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu
uamuzi wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu
ni kuwa watulivu mnapojadili suala hili.
Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi.
Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi
kwa jambo hili una hasara kubwa. Tunaweza
kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama
kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania
inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na
matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa
Wajumbe; Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa
Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde
Warioba, mara kadhaa, mjadala au madai ya
kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo
jipya. Ulikuwepo hata wakati wa
mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu mbili
mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka
kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar mwaka
1984. Muundo huu uliwahi kupendekezwa na
Tume ya Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya
G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na
Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998. Lakini
mara zote hizo mapendekezo hayo
hayakukubaliwa. Waasisi wa taifa letu, yaani
Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa
Jamhuri ya Tanganyika wakati ule na Sheikh
Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule,
waliamua kuchagua Muungano wa Serikali
mbili tulionao sasa. Walitoa sababu mbili
kuu: “ni muundo unaoihakikishia Zanzibar
kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia
unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo
mkubwa wa kugharamia Serikali ya
Tanganyika na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Natambua kuwepo
kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere
asitumiwe katika mjadala huu. Nionavyo
mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za
Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume katika
jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na
kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili
ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje leo
tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao
yawe hayafai kutumika au hata
kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani
pekee ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa
hatuutendei haki mjadala huu na sisi
wenyewe tunaoshiriki katika mchakato huu.
Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja
zote kwa marefu na mapana yake ili mpime
kama zipo sababu za kuubadili muundo wa
sasa wa Muungano wa Serikali mbili na
kuleta wa Serikali tatu. Na, kama zipo
mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye
uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye
mashiko. (you must make an informed
decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti; Tume imetoa
sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo
wa Serikali tatu. Sababu ya kwanza ni
kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania
wengi kote Zanzibar na Tanzania Bara.
Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania
waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa
kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo
wa Serikali ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa
kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono
muundo wa Serikali tatu. Sababu ya pili ni
kwamba muundo huo unatoa majawabu ya
uhakika na endelevu kwa changamoto za
muundo wa sasa wa Serikali mbili
zinazonung’unikiwa na watu wa pande zetu
mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Sababu hizi mbili
kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala
mkali katika jamii. Wapo wanaokubaliana na
Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo
wanaosema Tume imesema kweli kwamba
Watanzania wengi wanaunga mkono muundo
wa Serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali
tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi
hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi
wape uheshimiwe. Lakini wapo wanaodai
kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli
huo. Wanasema kuwa taarifa ya Tume
imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni
yao kwa Tume kwa mdomo na maandishi
walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi
47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo
waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo
wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa
na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao
halikuwa tatizo, ndiyo maana
hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa
iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote
waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo
Watanzania walio wengi! Mheshimiwa
Mwenyekiti; Wanasema pia, kwamba mbona
Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu
(uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati ya
hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu
Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa
na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa
Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali
mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya
Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza
Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi
kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti; Takwimu za Tume
(uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume
ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo
asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia
muundo wa Muungano na asilimia 88.6
hayakuzungumzia Muungano bali mambo
mengine. Hivyo basi wanahoji pia kwamba
kama muundo wa Muungano ungekuwa ni
jambo linalowakera Watanzania wengi,
lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa
maoni na kwenye idadi ya maoni
yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza.
Waliouzungumzia Muungano walikuwa
asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa
maoni na maoni yanayohusu Muungano
yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo
basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya
Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko
wapi?” Changamoto za Muundo wa Serikali
Mbili Mheshimiwa Mwenyekiti na
Waheshimiwa Wajumbe; Kama
nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili
ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa kwa
muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo
huu unajibu changamoto nyingi za muundo
wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri
changamoto za muundo wa Serikali mbili.
Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile
kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo
kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano
kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar
hainayo. Aidha, wanasema mipaka na
mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa
mambo ya Muungano, na kwa mambo ya
Tanzania Bara haijaainishwa vizuri
ikaeleweka. Wazanzibari pia, wanazungumzia
mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato,
na jinsi ya kuchangia shughuli za Muungano
baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile,
wanalalamikia Rais wa Zanzibar kuondolewa
kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano. Aidha, kuna malalamiko kuwa
orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa
kutoka mambo 11 mwaka 1964 mpaka 22
mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar
kwa mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa upande wa
Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa
manung’uniko kuwa Muungano wa Serikali
mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria
wa Tanganyika na fursa ya watu wa upande
wa Tanzania Bara kutetea maslahi yao ndani
ya Muungano. Wanasema Zanzibar sasa
imekuwa nchi huru; ina bendera yake, wimbo
wake wa taifa na Serikali yake. Aidha,
wanasema Zanzibar imebadili Katiba na
kujitambulisha kama nchi na kuchukua
madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile
Sheria zinazotungwa na Bunge lazima
zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi
kupata kibali cha kutumika Zanzibar.
Wananchi wa Tanzania Bara pia
wanalalamikia kutokuwa na haki ya kumiliki
ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka
Zanzibar wanayo haki hiyo Tanzania Bara.
Na wao vilevile wananung’unikia
mkanganyiko kuhusu ugawaji wa mapato na
jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa
shughuli za Muungano baina ya Serikali ya
Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hizi ndizo
baadhi ya changamoto ambazo Tume inaona
jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo
wa Muungano kuwa wa Serikali tatu badala
ya mbili za sasa. Faida za Muundo wa
Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti; Tume ya Mabadiliko
ya Katiba imefafanua kwamba mfumo wa
Serikali tatu utagawanya vizuri madaraka kati
ya mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha
Washirika wa Muungano kubaki na
utambulisho wao wa kihistoria na
kiutamaduni na hivyo, utawezesha kuondoa
hisia za Zanzibar kumezwa na Muungano.
Pia unawezesha kila upande wa Tanzania
kuendesha mambo yake yasiyo ya Muungano
kadri wanavyoona inafaa. Vile vile unaweza
ukaleta ushindani wa kimaendeleo baina ya
washirika na hivyo kusaidia kukuza
maendeleo ya nchi. Faida za Muundo wa
Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti; Pamoja na
kuainisha changamoto za muundo wa
Serikali mbili na kupendekeza kuwa muundo
wa Serikali tatu ndio utakaosaidia kuzitatua,
Tume haikuacha kutambua manufaa na
mchango muhimu uliotolewa na muundo wa
Serikali mbili kwa nchi yetu. Tume inasema
kuwa muundo wa Serikali mbili unapunguza
gharama za uendeshaji wa shughuli za
umma. Umesaidia kujenga uhusiano na
ushirikiano mzuri katika nyanja mbalimbali
baina ya wananchi wa pande zetu mbili za
Muungano. Umezuia mkubwa kummeza
mdogo; na umedumisha Muungano mpaka
kuufikisha hapa ulipo tangu kuasisiwa kwake
takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha,
umesaidia kudumisha amani, umoja na
utulivu hapa nchini. Changamoto za Muundo
wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti; Pamoja na kuelezea
ubora wa muundo wa Serikali tatu kama
jawabu kwa changamoto za Serikali mbili,
Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una
changamoto zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya
Tume inaeleza kuwa kutakuwa na gharama
kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma.
Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba alitutoa
hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993,
Mwalimu alikuwa na mawazo tofauti.
Alisema kwamba: “watu …wanaodhani kuwa
gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo
ingekuwa ndogo, (Waulizeni Wazanzibari) na
wala gharama ya Serikali ya Shirikisho
isingekuwa ndogo hata bila gharama ya
mambo yasiyo ya Shirikisho”. Ni matumaini
yangu kwamba katika mjadala wenu mtajipa
nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa na
nyeti. Tume imesema pia kwamba, Muundo
huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji wa
gharama za uendeshaji wa shughuli za umma
baina ya nchi washirika. Vilevile, kuna
uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au
kutofautiana juu ya masuala ya msingi ya
nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika wa
Muungano na baina ya nchi washirika na
Serikali ya Muungano. Aidha, upo uwezekano
mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti za
kimaendeleo baina ya pande mbili za
Muungano kutokana na kila upande kuwa na
sera na mipango tofauti. Tume pia imeelezea
hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza
hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa
nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha
Muungano. Muundo huu pia unaweza kuleta
misuguano (paralysis and deadklocs in
decision making) katika kufanya uamuzi juu
ya masuala muhimu ya kitaifa. Changamoto
hizo si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi
wa Muungano bali pia hata uhai wake. Kwa
ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu
kuna maana ya kufanya kazi ya ziada ya
kuzikabili changamoto hizi ili zisiue
Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si
ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Wanaounga mkono
muundo wa Serikali mbili wanasema kuwa
kwa mlolongo huu wa changamoto
zilizoainishwa na Tume yenyewe,
unadhihirisha kuwa muundo wa Serikali tatu
hautapunguza matatizo ya Muungano wetu
bali utayaongeza maradufu kuliko ilivyo sasa.
Wanakiri kuwepo kwa changamoto katika
muundo wa sasa wa Muungano. Hata hivyo,
wanaamini zinaweza kushugulikiwa na
kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na
Serikali ya tatu. Wanatoa mifano kadhaa ya
jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia
changamoto za Muungano katika kipindi cha
uhai wake na mafanikio yaliyopatikana.
Katika kushughulikia kero za Muungano,
Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya
Shelukindo mwaka 1992 na Kamati ya
Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka 1993.
Mambo mengi yaliyoainishwa katika Tume ya
Shelukindo na Kamati ya Pamoja
yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wa kero zilizoelezwa kwenye
Tume ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006
yalikuwa yamebakia mambo 13 kati ya 31.
Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya
Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi sasa
yamesalia mambo sita tu. Kimsingi ni
mambo yahusuyo maslahi ya kiuchumi na
yote yapo katika hatua nzuri za kuyamaliza.
Mambo hayo ni: 1. Mgawanyo wa mapato:
(a) Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya
Sarafu ya Afrika Mashariki (b) Mgawanyo wa
Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu. 2.
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
3. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
4. Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika
taasisi za Muungano. 5. Usajili wa vyombo
vya moto. 6. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Serikali zetu mbili
zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya
mchakato huu wa mabadiliko ya Katiba
kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa
kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Mambo hayo ni matatu yafuatayo:
1. Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi
asili. 2. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi
za nje. 3. Tume ya Pamoja ya Fedha. Matatu
mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu
za kiutawala. Hali kadhalika, katika kipindi
cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani
2015 – 2018 ni nafasi nzuri ya kushughulikia
masuala yenye migongano kati ya Katiba ya
Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano.
Mimi naishi kwa matumaini na kwa vile
tunayo dhamira njema ya kuimarisha
Muungano wetu, naamini tutaweza kuziondoa
tofauti zilizopo. Orodha ya Mambo ya
Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kuhusu orodha ya
mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11
ya awali, napenda kuwahakikishia kuwa
Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar hazina kigugumizi
wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya
kuyapunguza yale yanayopunguzika.
Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa
kilichoongeza orodha hiyo si hila za Serikali
ya Muungano kutaka kupunguza madaraka
ya Zanzibar kwa mambo yake ya ndani. Na,
wala siyo udhaifu wa viongozi wa Zanzibar
katika kutetea maslahi ya nchi yao. La
hasha. Pili, naomba ieleweke kuwa, kila
kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya
Muungano kilikuwa na sababu inayoeleweka,
inayoelezeka na iliyokubalika na pande zote
mbili za Muungano. Hakuna hata jambo
moja lililoingizwa kwenye Katiba kwa kificho.
Taratibu stahiki za kikatiba na kisheria
zilifuatwa. Hoja ziliwasilishwa Bungeni na
kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi ulifanywa na
Bunge kwa kuzingatia kanuni ya theluthi
mbili ya kura za kila upande wa Muungano.
Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge
la Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila mtu
anayetaka kuzisoma asome. Nashauri
mkazisome ili mpate kujua ukweli na undani
wa kila kilichoongezwa na sababu za kufanya
hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Nchi zetu mbili
zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, kulikuwa na
mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
Mambo ya Nje,
Ulinzi,
Polisi,
Hali ya Hatari,
Uraia,
Uhamiaji,
Biashara ya nje na mikopo,
Utumishi katika Serikali ya Muungano,
Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru
wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kati ya mwaka 1965
na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka
kutoka 11 hadi kufikia 22, kimsingi kutokana
na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na
kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki.
Pande zetu mbili za Muungano zilikubaliana
kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba
na taratibu za kisheria na Kikatiba zilifuatwa.
Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo kwa
ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu
kilichosababisha mabadiliko hayo kufanywa.
Jambo la kwanza kuongezwa, yaani la 12
lilikuwa ni “sarafu, mabenki na fedha za
kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965
kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya
Afrika Mashariki (East African Currency
Board) mwaka 1964. Kwa ajili hiyo, kila nchi
mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa
na sarafu yake na mipango yake ya
kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha.
Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala
hayo yashughulikiwe na Serikali ya
Muungano na Muswada husika wa Bunge
uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee Abeid
Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais
tarehe 10 Juni, 1965. Tarehe 11 Agosti, 1967
yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano:- (a) Leseni
za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13) (b)
Elimu ya Juu, (Jambo la 14) (c) Jambo la 15
lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye
Nyongeza ya 10 ya Mkataba wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na
mambo 27 ambayo Serikali ya Muungano
ilipewa jukumu la uratibu. Mambo hayo ni
pamoja na Mahakama ya Rufani ya Afrika
Mashariki, Utabiri wa Hali ya Hewa, Utafiti,
Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli,
Barabara, Usafiri wa Majini na kadhalika.
Tarehe 22 Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta,
petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa
jambo la 16. Kimsingi Serikali ya Muungano
ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli
na gesi asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada
ya kupanga upya Orodha ya Mambo ya
Muungano, suala la rasilimali ya mafuta
likawa la 15. Tarehe 22 Novemba, 1973
Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na
kuwa jambo la 16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa
Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka
1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda
Baraza la Mitihani la Taifa mwaka 1973.
Mwaka 1984 yalipofanyika mabadiliko
makubwa katika Katiba ya mwaka 1977,
Orodha ya Mambo ya Muungano ilipangwa
upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye
Nyongeza ya 10 ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la
15 katika Orodha ya Mambo ya Muungano
yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo
hayo yalipewa namba kama ifatavyo:-
Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17,
Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa
kuwa la 19 na Takwimu kuwa la 20 na
Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa
jambo la 21.
Tarehe 17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la
“Uandikishaji wa Vyama vya Siasa” na kuwa
jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa
Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na hasa
uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Bila ya shaka
maelezo haya yatasaidia kuelezea nini
kimeongezwa na mazingira ya kuongezwa
kwake ni yepi. Kulikuwepo na sababu za
msingi na wala siyo hila ya namna yo yote
ile iliyofanywa na mtu ye yote mwenye nia
mbaya na Zanzibar. Kama tulivyoona mambo
mengi yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kila
yalipotokea mabadiliko katika uendeshaji wa
shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki,
huduma zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya
zilikabidhiwa Serikali ya Muungano kubeba
kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa
kiuchumi. Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu
zetu mbili za Muungano yaliingizwa katika
Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo
yaliachiwa kila upande kushughulikia
ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo
ambayo yalitokana na uamuzi wetu wenyewe
ni mawili tu. Mambo hayo ni rasimali ya
mafuta na gesi asilia (1968), na uandikishaji
wa vyama vya siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti; Ni msimamo wa
Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo
kwamba, iwapo Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa
kufanya baadhi ya mambo katika Orodha ya
Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa
kufanya hivyo. Lililo muhimu ni kuwa
zisiondolewe tunu zenyewe za Muungano
wetu. Ndiyo maana, mambo kama vile
bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni za
biashara, utafiti na mengineyo,
yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwemo
kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa sasa na
imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni
makusudio yetu kutumia fursa ya mchakato
huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na
mengineyo tutakayokubaliana kutoka kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano. Rasilimali
ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa ajili hiyo
tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali
ya mafuta na gesi asilia lisiwe jambo la
Muungano. Jambo hili tulishakubaliana
tangu wakati wa Rais Amani Abeid Karume
tuliondoe na hata alipokuja Rais Shein
msimamo haukubadilika. Kilichotuchelewesha
kutekeleza ni kuibuka kwa fikra za kuwa na
mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona
kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria wa
kuondoa jambo hili katikati ya mchakato huu,
ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa ya
lazima. Tungeulizwa haraka ni ya nini
tungeweza kukosa majibu. Hatimaye wakati
wake wa kulimaliza suala hili sasa umefika.
Misemo ya wahenga ya “subira yavuta heri”
na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika
mahali tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu
mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa
rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano. Kwanza kwamba, siku hizi
Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa
na makampuni binafsi. Pili, kwamba,
rasilimali ya mafuta na gesi yakipatikana
Zanzibar ni suala la kiuchumi ambalo lipo
kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo
karafuu, hiliki, mwani na kadhalika. Au kama
ilivyo dhahabu, gesi, pamba, kahawa na
kadhalika kwa upande wa Tanzania Bara.
Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali
yake ya kiuchumi. Zanzibar na Ushirikiano wa
Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti; Jambo lingine
muhimu ambalo Serikali zetu mbili
zimelizungumza na kukubaliana tulitafutie
ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya
kujiunga na mashirika ya kimataifa, kukopa
na kupata misaada kutoka nchi za nje bila
kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo vya
namna mbalimbali. Ni ukweli usiopingika
kuwa jambo hili limechangia kwa kiasi
kikubwa kujenga hisia hasi kuhusu
Muungano kwa upande wa Zanzibar. Aidha,
limechangia sana kuchafua hali ya hewa ya
kisiasa Zanzibar kwa nyakati mbalimbali.
Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara
imejificha kwenye koti la Serikali ya
Muungano, na kutaka itoke ionekane ili iache
kunufaika isivyostahili, zinazochangiwa sana
na mazingira haya iliyonayo Zanzibar.
Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo
haya yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa
tumeondoa kizingiti kikubwa katika ustawi
wa Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar tumekubaliana kuwa,
tutumie fursa za mchakato huu kuyamaliza
mambo haya yaishe! Bahati nzuri dhana
iliyopo katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu
inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili.
Tukikubaliana, itaipa Zanzibar “uwezo na
uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano
na jumuiya au taasisi yo yote ya kikanda na
kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya
mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya
nchi” bila kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu
mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa kwa
Zanzibar bila ya kulazimika kuwa na muundo
wa Serikali tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Kwa maoni yangu
kitu kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza
msukumo, utakaohakikisha kuwa Tume ya
Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo
majukumu yake. Wanaohusika na utekelezaji
wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo
kutimiza wajibu wao. Iwekwe mifumo na
masharti katika sheria au Katiba ya
kuwabana watekelezaji kwa ajili hiyo. Hali
kadhalika ihakikishwe kuwa, Akaunti ya
Pamoja inaanzishwa bila ajizi na kutumika
na pande zote. Aidha, mfumo wa
mawasiliano na ushirikiano baina ya Serikali
zetu mbili yaani Kamati ya Pamoja ya
Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria
na kama hapana budi upewe nguvu ya
Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa
kuyaweka mambo yote sawa hata bila ya
kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Waheshimiwa
Wajumbe; Katika mjadala kuhusu
mapendekezo ya kuwa na muundo wa
Muungano wenye Serikali tatu, wananchi
wametoa maoni na mapendekezo mengi
mazuri kuhusu changamoto za Serikali tatu
zilizoainishwa na Tume na namna ya
kuzitatua. Tena yapo maoni ya watu
wanaopenda muundo wa Serikali tatu na
wasiopenda muundo wa Serikali tatu.
Nawaomba myatafakari kwa uzito
unaostahili. Yapo mambo muhimu ya
kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa mfano ni
ile hoja kwamba Serikali ya Muungano
inayopendekezwa haikujengeka kwenye
msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe za
kusimama. Inategemea mno ihsani ya nchi
washirika. Kwa sababu hiyo inaweza
kuanguka wakati wowote, na Muungano
kusambaratika, iwapo itakosa ihsani ya nchi
washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata
kama ni mmoja wa washirika amefanya
hivyo. Pili, kwamba, haielekei Serikali hiyo
ina chanzo cha uhakika cha mapato ya
kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza
majukumu yake. Ushuru wa bidhaa
unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa
hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba,
hakuna uhakika wa fedha hizo kupatikana
kwa vile, Serikali ya Muungano haina chombo
chake chenyewe cha kukusanya mapato hayo.
Itategemea vyombo vya nchi washirika
kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya
shughuli za Serikali ya Muungano kusimama
wakati wo wote au hata kusimama kabisa
kwa sababu ya nchi washirika kuchelewa au
kushindwa kuwasilisha makusanyo ya kutoka
kwao. Bahati mbaya Serikali ya Muungano
haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha
kuwa mapato yake yanawasilishwa. Serikali
hiyo haina mamlaka ya kuzibana nchi
washirika kuwasilisha au kuziwajibisha
zisipofanya hivyo. Katika mazingira hayo ni
rahisi kwa Serikali ya Muungano kukwama na
kushindwa kutekeleza majukumu yake. Huu ni
muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa
Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Katika Rasimu ya
Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa
ya kukopa kama chanzo cha kujipatia mapato
ya kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa
sababu ya kukosa rasilimali zake yenyewe,
huenda ikawa vigumu kwa Serikali hiyo
kukopesheka. Kwa jumla hii ni Serikali
ambayo ukuu wake hauna nguvu iliyo thabiti,
na watu wengine wanaona kama vile ukuu
huo haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye yote
wa nchi washirika akatunisha misuli dhidi ya
Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya
Serikali au chombo cha Muungano, Rais na
Serikali yake watakuwa hawana lo lote la
kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika
muundo wa Serikali tatu ni wa mashaka
makubwa. Hofu hizi kuhusu udhaifu wa
Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa
Serikali tatu unaopendekezwa, zinawasumbua
hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali
tatu kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali
ya Muungano yenye nguvu na inayoweza
kusimama yenyewe kwa kujitegemea.
Wanaona kilichopendekezwa hakitoi
matumaini hayo. Hii ina maana kuwa lazima
mawazo bora zaidi yatolewe ili kupata
Serikali ya tatu yenye ukuu unaoonekana na
inayoweza kusimama yenyewe bila kuwa
tegemezi na egemezi kwa nchi washirika. Pia
inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi
washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua
tufuate mfumo huo linaweza kuonyesha njia
ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa
Serikali mbili wanaona kuwa huu ni
uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali
mbili. Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti; Katika kuainisha
changamoto za muundo wa Serikali tatu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeyataja
mambo mengine mawili makubwa ambayo
ningependa Waheshimiwa Wajumbe muyape
tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi,
misuguano na mikwamo (deadlocks and
paralysis) katika kujadili na kufanya uamuzi
kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na
pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa
(nationalistic sentiments) wa zamani kwa
nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa
makini sana mambo haya, kwa sababu ya
uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu
ustawi na uhai wa Muungano, bali hata
usalama wa raia na mali zao. Naona hata
Tume haikuweza kupata ufumbuzi ulio
mwafaka kabisa kwa changamoto hizi. Bila
ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa
Wajumbe mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Ni lazima lifanyike
kila linalowezekana kuhakikisha kuwa
maamuzi hayakwami kwani yakikwama
maana yake shughuli za Muungano zitakuwa
zimekwama. Kama hazitakwamuliwa kwa
wakati ustawi wa Muungano utaathirika.
Ikishindikana kabisa kupatikana ufumbuzi
Muungano unaweza kuvunjika. Kuibuka na
kukua kwa hisia za utaifa (nationalistic
feelings) kwa nchi washirika, yaani
Utanganyika na Uzanzibari ni tishio kubwa
sana kwa uhai wa Muungano. Hebu fikiria,
watu walioishi pamoja kidugu na kwa
kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa
nchi moja yaani Watanzania kwa miaka 50,
kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya
Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya
Watanznaia. Kwa mujibu wa sensa iliyopita
takriban asilimia 90 ya Watanzania waliopo
sasa wamezaliwa baada ya mwaka 1964.
Nchi wanayoijua ni Tanzania. Litakuwa ni
jambo lenye mshtuko mkubwa na athari
zisizoweza kutabirika, watu hao
watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa
kutengenezewa utaratibu maalum wa kusafiri
na kuishi wakiwa upande wa Muungano
ambao siyo kwao kwa asili. Wanakuwa
wageni na fursa walizokuwa wanazipata
waendapo popote haiwi rahisi tena kuzipata.
Katika mazingira hayo ni rahisi sana chuki
kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu
mara moja watajikuta maadui. Aidha, watu
wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi kwao
kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa sababu
ya mazingira kuwa magumu kiasi cha kuona
bora waondoke. Watu hao wanaweza
kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma
kila kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Changamoto hizi
kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu
ambazo Tume imeziona, ni za kweli. Si
mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu
wenye asili ya Tanzania Bara ya kuchomewa
moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na
watu wenye hisia kali za Uzanzibari, na
kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar,
huenda yakawa madogo. Matukio ya namna
hii yanaweza kutokea pande zote mbili na
kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina
ya watu, baadaye itakuwa baina ya Serikali
zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu mbili
zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne,
ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na
wasiotakiana heri. Umoja wetu utatetereka na
Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini
tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti; Sisi viongozi
tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya
wananchi wetu, hatuna budi kuyapima
mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye
uamuzi ulio sahihi. Tusije tukajutia uamuzi
wetu tutakapoona watu wanafukuzana,
wanauana na mali zao kuporwa. Na, tukifikia
hatua hiyo Muungano kusambaratika
halitakuwa jambo la ajabu. Kwa kweli,
unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa
nini wazee wetu waasisi waliamua
walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra
zao na maono yao. Kuna hatari ya nchi yetu
na watu wake kupoteza kila kitu
tulichokijenga kwa miaka 50. Badala ya
kujenga tunaweza kujikuta tumebomoa hata
msingi katika nchi washirika. Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1993
alituasa kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi
kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila
adhabu… na adhabu nyingine zimo mle mle
ndani ya kitendo hazisubiri.” Mheshimiwa
Mwenyekiti; Siku moja kiongozi mmoja wa
juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza:
“Hivi Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu
ni kuongeza ya tatu? Si matatizo ndiyo
yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo
Serikali tatu si kila mtu atachukua njia yake?
Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi
nawashauri msichoke kutafuta majawabu kwa
matatizo ya hizi mbili! Huko mnakotaka
kwenda kuna hatari nyingi”. Pengine na
ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema
kuupa nafasi na kuutafakari. Kazi Yenu
Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti; Mambo ya
kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu
ya ufinyu wa muda, nisingeweza
kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona
katika kuipitia Rasimu na kwenye majadiliano
yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi
iliyo mbele yenu ni kubwa sana. Ni kubwa
kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe la
kutunga Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira
ya nchi yetu itakuwaje na itaendeshwa vipi
kwa miaka mingi ijayo iko mikononi mwenu.
Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili, ni kubwa
kwa maana ya uzito wa mambo ya kujadili
na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni
muhimu sana kuisoma Rasimu na Taarifa ya
Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni muda
wa kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila
dhana ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi.
Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi
yetu na Watanzania wote kupata Katiba
nzuri. Nimefarijika sana kusikia kuwa
mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa
kujadili Rasimu. Huu ni utaratibu mzuri kwani
mkiwa katika vikundi vya watu wachache,
mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu
wote wanaweza kupata fursa ya kutoa maoni
yao, kwa kila kifungu na kila jambo
linaloibuliwa na kuzungumzwa. Kwa kufanya
hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu
la kutunga Katiba. Wote mtakuwa mmeshiriki
kujadili kila sura na vipengele vyake vyote.
Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki sifa
nzuri kama Katiba itakuwa nzuri, au lawama
stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti; Nitakuwa mwizi wa
fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya
kutambua kazi nzuri iliyofanywa na
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa
Baraza la Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti
wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake haikuwa
rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na
ustadi mkubwa ameweza kufanikisha mambo
kwa kiasi ambacho anastahili pongezi zetu
sote. Anastahili pongezi kwa sababu yeye
aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo kwa
kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti
wa Kudumu kaka yangu Mheshimiwa Samuel
Sitta. Napenda pia kuwapongeza
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba kwa hatua mliyofikia. Hata hivyo,
mmechukua muda mwingi katika hatua ya
awali hivyo hamna budi kuongeza kasi.
Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu
hii inafuatiliwa kwa karibu sana na
Watanzania. Wamewekeza sana matarajio
yao kwenu. Hamna budi, haiba na taswira ya
uongozi muionyeshe wakati wote wa
kuendesha mijadala yenu kwa lugha na
vitendo vyenu. Wakati wa semina na mjadala
wa kupitisha Kanuni za Bunge hili, baadhi ya
wananchi wamekwazika sana na mwenendo
wa baadhi ya Wajumbe. Hawakutegemea
kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya na
kusikia maneno waliyoyasikia kutoka kwenye
vinywa vya baadhi yenu. Ni matumaini yangu
na ya Watanzania wote kuwa hali ile
haitajirudia tena katika awamu hii.
Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata
tamaa na Wajumbe wao au na hata chombo
hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na
wa nchi yao. Tutoe hoja badala ya kupiga
kelele (argue don’t shout) au kuzomea.
Hakuna haja ya kutumia lugha isiyokuwa ya
staha katika kujieleza. Hakuna haja ya
kukingiana ngumi, kutishiana hili na lile au
hata kugombana. Ni utovu wa uungwana
usiotegemewa kutoka kwenu. Tusiwaangushe
wananchi wa Tanzania wanaotutegemea
sana. Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti; Ombi langu la
mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa wakati wote
muongozwe na kujali maslahi mapana ya
nchi yetu na watu wake badala ya kujali
maslahi yenu binafsi au ya makundi yenu.
Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania
Kwanza”. Najua kila mmoja wenu amekuja na
maoni yake au atakuwa nayo kwa kila jambo
litakalojadiliwa. Wengine wamepewa
misimamo na vyama vyao au makundi yao.
Si jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta
mafanikio, kama misimamo hiyo na mawazo
hayo ni ya kujenga. Hata hivyo,
mnachotegemewa kufanya ni kuwa tayari
kuwianisha na kuunganisha mawazo yenu
mazuri na ya wenzenu, ili kupata msimamo
wa pamoja na uamuzi wa pamoja ulio bora.
Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari
kusikiliza mawazo ya wengine, hata kama ni
tofauti na yenu mliyokuja nayo. Tafuteni
kilicho chema kwa yale yanayosemwa na
watu wengine hata kama ni watu
usiokubaliana nao au huwapendi au
hampendani. Kunaweza kuwepo kitu chenye
manufaa. Mheshimiwa Mwenyekiti na
Waheshimiwa Wajumbe; Nawaomba muwe
hodari wa kushawishi badala ya kulazimisha.
Mkifanya hivyo hamtalazimika kutumia muda
mwingi wa kula njama za namna ya kuwazidi
maarifa wale mnaotofautiana nao kwa
mawazo. Lazima pia mtafute namna ya
kushirikiana na kuwasiliana na makundi
mengine. Msitafute kushindana, hili ni jambo
ambalo lazima wote mtoke hapa mkiwa
washindi. Yaani lazima Watanzania wote
washinde kwani wao ndiyo wenye Katiba yao.
Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa
na asasi mbalimbali kwa kutambua na
kuthamini umuhimu wa kuwa na taratibu za
mawasiliano, mashauriano na ushirikiano.
Daima muwe watu wa kutafuta maridhiano.
Mmefanya vizuri katika hatua ya awali.
Mmejiwekea taratibu nzuri za kufanya hayo,
tafadhalini zitumieni. Jengeni madaraja
imara zaidi katika awamu hii. Mheshimiwa
Mwenyekiti; Naomba nimalize kwa kuwaomba
Watanzania wote tukiongozwa na viongozi
wetu wa dini tumuombe Mola wetu ajalie
rehema zake ili mchakato wa kutunga Katiba
uende salama. Aliongoze Bunge hili na
Wajumbe wake waweze kufanya uamuzi ulio
sahihi na wenye manufaa kwa taifa letu kwa
kila watakaloliamua. Baada ya kusema
maneno yangu mengi hayo, nirudie
kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa
kunipa fursa hii adhimu ya kulihutubia Bunge
Maalum la Katiba. Nawatakieni kila la heri na
mafanikio mema. Katiba Mpya Inawezekana,
Timiza Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Tanzania! Mungu Libariki
Bunge Maalumu la Katiba! Asanteni sana
kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment