Na Evarista Lucas
Singida ,
Desemba 21,2013
Askari wa Jeshi la Polisi Mkoani Singida Zakaria
William mwenye namba D.6466 D/SGT
amepoteza maisha papo hapo mapema jana baada ya kupigwa risasi iliyopenya
shingoni mwake na mtu anayesadikiwa ni jambazi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mapema leo katika
ofisi yake; Kamanda wa Polisi mkoani Singida Bwana Geofrey Kamwela amesema
tukio hilo la kusikitisha limetokea majira ya saa nne na nusu za usiku katika kijiji cha Tambukareli katika
kata ya Majengo iliyopo wilayani Manyoni mkoani hapa.
Kamanda Kamwela ameeleza kuwa; tukio hilo limetokea wakati askari huyo
akiwa katika doria na askari wenzie
walipopata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa katika nyumba moja ya mali ya
Stanley Mpaki (Almaarufu kama Babu Mpaki) mfanyabiashara na mkulima anaishi na
watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
Baada ya kupata taarifa hizo marehemu na wenzie walifika
katika nyumba hiyo ambapo baadhi ya
askari waliingia ndani ili kuwakamata watuhumiwa na marehemu alikuwa amebaki nje ambapo alipigwa
risasi na mmoja kati ya majambazi hao aliyetoroka kusikojulikana na kupoteza
maisha papo hapo.
Katika nyumba hiyo watu wanne wamekamatwa ikiwa ni
pamoja na bunduki aina ya SMG yenye namba UA ikiwa na risasi ishirini na tano
ndani ya magazine moja na bastola moja ya kienyeji yenye uwezo wa kutumia
risasi za shotgun pamoja na risasi saba.
Aidha; Kamanda Kamwela amewataja majambazi
waliokamatwa ktika tukio hilo ni pamoja
na Joseph Hemed mwenye umri wa miaka ishirini na tisa mkulima na mkazi wa
Siuyu, Ikungi; Juma Ramadhan miaka ishirini mkulima na mkazi wa Kizota, Dodoma;
Abdallah Hamis ini na moja, miaka ishirmkulima na mkazi wa Milera Ikungi na Stanley
Mpaki miaka ishirini na minane mkazi wa Itigi ambao walitambuliwa kuwa ni
wahalifu wazoefu kutokana na kuhusika kwao katika matukio mbali mbali ya
uhalifu wa kutumia silaha.
Sanjari na hayo Kamanda Kamwela amesema Jeshi la
polisi Mkoani hapa linaendelea na uchunguzi wake juu ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kumsaka mtuhumiwa
aliyetoroka na uchunguzi utakapoakamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida hili ni tukio la pili ambalo
limepelekea askari wake wawili kupoteza maisha wakiwa kazini, ambapo askari wa
kwanza alipoteza maisha katika
oparesheni tokomeza majangiri huko Manyoni baada ya kushambuliwa na majangiri.
Kwa upande mwingine
Kamanda Kamwela amesema umilikaji silaha kinyume cha sheria ndiko
kunakopelekea kuibuka kwa vitendo vya ujambazi na kuwashukuru raia wema wote ambao wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na kuongeza
kuwa uhai wa askari marehemu Zakaria umepotea kutokana na silaha haramu.
Pia; Kamanda Kamwela
ametoa wito kwa wananchi wote kuendelea
na moyo wa kutoa taarifa kwa Jeshi la polisi na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama kuhusu uhalifu au wahalifu na matishio mengine ya usalama ili
yafanyiwe kazi haraka na kuepusha madhara kwa watu na mali.
No comments:
Post a Comment