Advertssssss

Advertssssss

Menu drop

Sunday, December 29, 2013

UFAULU WA WANAFUNZI DARASA LA SABA SINGIDA WAONGEZEKA

Na   Evarista Lucas
Singida
Desemba 28, 2013

Imeelezwa kuwa; kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi waliohitimu darasa la saba mwaka 2013 kimeongezeka kwa asilimia 17.56 ikilinganishwa na kiwango cha ufaulu cha asilimia 23.16 kwa mwaka 2012.

Hayo yamesemwa mapema leo katika kikao cha bodi ya uchaguzi wa wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza mwaka 2014; na Afisa Elimu mkoa wa Singida Bibi Fatuma Kilimia wakati akiwasilisha muhtasari wa matokeo ya darasa la saba  mwaka 2013 mapema leo katika ukumbi wa RC Mission mjini Singida.

Aidha Kilimia ameongeza kusema kuwa, licha ya kuongezeka kwa kiwango hicho cha ufaulu kwa asilimia 17;  bado kuna changamoto zinazoikabili sekta ya elimu na kuathiri utoaji taaluma bora hapa mkoani.

Amesema, ili kuzikabili changamoto hizo; sekta ya elimu imeazimia kuendesha mafunzo ngazi ya Klasta na Kata ya masomo yenye utata na kusoma, kuandika na kuhesabu kwa kutumia njia ya ‘Lesson Study’ kwa kutumia Walimu bingwa,na  kubaini Walimu Wakuu wasiowajibika ipasavyo na kuwavua Madaraka.

Sanjari na hayo ni Halmashauri kuwawezesha Wakaguzi ili shule zikaguliwe kwani ukaguzi ndiyo kioo cha taaluma na pia kusikiliza na kutatua kero za Walimu.

Kwa upande mwingine imefahamika kuwa walimu wengi wamekuwa hawafanyi kazi zao kwa ufasaha kutokana na changamoto mbali mbali zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku na kubwa zaidi ikiwa ni madeni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajumbe wakikao hicho  cha bodi ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2014 wamesema; walimu wengi wamezidisha mikopo hali inayowafanya washindwe kufanya kazi ya ufundishaji kwa ufasaha kwa kutumia muda wao mwingi kuwaza namna ya kulipa madeni yanayowakabili.

Akichangia katika mada katika kikao hicho; mjumbe na mwenyekiti wa huduma za jamii Halmashauri ya wilaya ya Singida Bwana Elia Digha amesema ni jukumu la wakuu wa Wilaya na wakurugenzi kuhakikisha kuwa walimu wanafanya kazi yao ipasavyo na kuepuka mikopo mikubwa zaidi,

Digha amesema; walimu wengi wamekuwa wakichukua mikopo mikubwa ambayohuongezeka riba pale wanaposhindwa kulipa deni na kujikuta na deni kubwa kuliko kiasi walichokopa. Akisisitiza hilo; Digha amesema ukopaji huo hufikia hatua mbaya ya kuwalazimu walimu(Wakopaji) kuaccha kadi zao za Benki kwa wadeni wao kitendo kinachowaathiri hadi kwenye utendaji kazi wao.

Kwa upande  wake diwani wa Itigi Bwana Alli Minja  amesema ni suala la ukopaji ni la mtu binafsi na si kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwazuia kukopa, minja amesema kuwa walimu wengi wanaokopa ni kwa tamaa zao ni kuwa kuwazuia ni kazi ngumu labda kuwapeleka nyumba za ibada wakaombewe ili pepo hilo la ukopaji litoke.

Amesema , haitoshi kudhibiti viwango vya mikopo kwa walimu kutoka katika asasi mbali mbali za serikali kwaani bado kuna watu binafsi wanaondesha shughuli hiyo ya ukopeshaji na walimu hukimbilia huko kukopa.
 
MWISHO

No comments:

Post a Comment