Alhamis 9 Januari 2014
Singida.WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria kugongwa na kuburutwa na basi la kampuni ya Mtei Express ya mjini Arusha.
Watu hao ni Tamili Shaban na Kassimu wamefariki dunia papo hapo kwenye eneo la tukio ambalo ni kitongoji cha Ijanuka kijiji cha Kisasida manispaa ya Singida.Hamza amefariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa mjini hapa.Miili ya watu hao imehifadhiwa katika chumba cha mochwari katika hospitali ya mkoa.
Baba mzazi wa watoto hao,Shaban Bunku ambaye imedaiwa ni mlinzi wa kampuni ya TTCL mjini hapa,amelazwa katika hospitali ya mkoa na hali yake ni mbaya.Inadaiwa kuvunjika mguu wa kulia na damu zilikuwa zikimtoka kichwani.
Wanafamilia hao wanadaiwa walikuwa wakienda shamba kuendelea na palizi.
Akizungumzia tukio hilo la kusikitisha,kamanda wa polisi mkoa wa Singida,SACP,Geofrey Kamwela,alisema tukio hilo limetokea jana (9/1/2014) saa moja na dakika moja asubuhi huko katika kitongoji cha Ijanuka kijiji cha Kisasida.
Alisema siku ya tukio,basi la kampuni ya Mteni lenye namba za usajili T.742 ACU aina ya scania likiendeshwa na Dismas Ludovick,lilikuwa linatokea Singida mjini likielekea Arusha mjini.
Kamwela alisema lilipofika kitongoji cha Ijanuka,kwa pikipiki aina ya sky go T.368 BXZ iliyokuwa inaendeshwa na Shaban Bunku huku akiwa amepakia watoto wake wa kiume watatu,ilikatisha ghafla kitendo kilichosababisha kugongwa na kuburutwa zaidi ya hatua 20.
"Dereva wa basi hilo ambalo lilikuwa na abiria tisa,alilazimika kusimamisha basi hilo kutokana na kuburuta pikipiki hiyo.Baada ya kusimamisha basi hilo,wananchi wa eneo hilo walipigiana simu na ghafla walijaa na kuanza kuvunja vunja vyoo na kisha kilichoma moto",alisema Kamwela.
Basi la kampuni ya mtei likiteketea kwa moto baada ya kuchomwa na wananchi baada ya kusababisha ajali |
Muonekano wa basi la kampuni ya mtei baada ya kuchomwa moto na wananchi |
Wakati huo huo,Kamanda Kamwela alisema wameanzisha msako mkali wa kusaka wananchi waliojichukulia sheria mkononi ili kuwakamata waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
"Tabia hii ya kujichukulia sheria mkononi haikubaliki,tutahakikisha tumewakamata wote waliohusika na uharibifu huu.Sheria ipo wazi kwamba hata kama mtu kafanya kosa,wananchi hawaruhusiwi kabisa kujichukulia sheria mkononi",alifafanua.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment