Na Evarista Lucas
Jan 25,2013
Singida
MENEJA mikopo wa shirika la kuhudumia viwanda vidogo
(SIDO) mkoa wa Singida; Bwana Ruben Mwanja amewasihi wachukua mikopo ya SIDO
kutoitumia vibaya mikopo hiyo kwa kuongeza wake wengine au kuvunja ndoa za watu
bali itumike katika kuendeleza biashara zao na kujiongezea kipato.
Mwanja ameyasema hayo mapema juzi wakati akizungumza
kwenye hafla ya kukabidhi mikopo mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni
18.9 za kitanzania kwa wanachama 39 wa kikundi cha Urafiki cha Singida mjini.
Amesema; uzoefu unaonyesha wazi kwamba baadhi ya
wanawake wanaobahatika kupata mikopo,hukorofishanana au kutengana kabisa waume
zao kwa ajili ya mikopo hiyo.
Licha ya hayo;Mwanja,amewataka wajasiriamali hao kutumia
mikopo yao vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa,na pia mikopo hiyo isaidie
kuimarisha ndoa zao. Amesema; wapo baadhi ya wanaume wakishapata mkopo wa
kuendeleza biashara zao,hukimbilia kuoa mke mwingine.
Kwa upande wake meneja wa SIDO mkoa wa Singida Bwana
Shoma Kibenda; amekipongeza kikundi cha Urafiki kutokana na sababu kwamba kina utamaduni mzuri wa kurudisha
mikopo kwa wakati na bila matatizo.
Kibenda amewataka wanakikundi hao wapige hatua zaidi
kwa kuangalia uwezekano wa kuanzisha viwanda vidogo kama njia moja wapo ya
kujiongezea kipato zaidi.
Katika hafla hiyo; Mikopo iliyotolewa kima cha chini kilikuwa shilingi 300,000 na
cha juu,kilikuwa ni shilingi 500,000 kwa mwanachama mmoja mmoja ambapo riba ya
mikopo hiyo ni asilimia 1.8 kwa mwezi.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment